Sunday, March 18, 2012

MAANA YA NENO NAKUPENDA

Ujumbe  unatoka:  1Wakorintho 13:4-6
Upendo …haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli.
tAFAKARI:
Neno KUPENDA, au UPENDO, limekuwa msamiati mgumu sana kwa vijana wa leo, shetani amefanikiwa kwa asilimia 90 kuwanasa vijana wengi na kuwaangusha katika dhambi, akitumia msamiati huu NAKUPENDA. Nikiwa katika huduma zangu za Injili, nilikutana na binti mmoja ambaye alikuwa amezidiwa kitandani akiwa anaumwa, lakini pia alikuwa mja mzito. Nilipomuuliza mumewe yuko wapi, akaanza kulia, mwishowe akaeleza kisa cha kusikitisha jinsi kijana wa kiume alivyomdanganya kuwa anampenda, lakini baada kutimiza haja yake, akampiga “KIBUTI” hakutaka hata kumuona, alitelekezwa bila msaada.

Vijana wengi leo hasa wa kike wanaingizwa “CHAKA” wanadanganywa na vijana wa kiume kwa neno NAKUPENDA, Binti akiambiwa nakupenda, utamuona Macho na masikio yanaaza kulege, kusema ukweli wengi HAWAPENDI, bali WANATAMANI. Wengi wamepitia changamoto hiyo ya kuambiwa wanapendwa, lakini baadaye walijikuta hukana Upendo. Na matatizo ya ndoa nyingi za siku hizi yanatokana na mwanzo wa mahusiano kuwa ni kukidhi TAMAA ya mwili. Misukumo na Mihemuko ya Tamaa za NGONO imechukuliwa na Vijana wengi kuwa ni Upendo. Utakuta kijana wa kiume anaonyesha hisia zote za kupenda, yuko tayari kukupigia magoti, kukulamba miguu, kukupatia chochote utakacho, ili mradi akuonyeshe kuwa anakupenda. Kisa cha Amnoni na Tamari katika biblia “1Samweli 13:1-22”, kinaeleza jinsi Amnoni alivyougua kwa kumpenda dada yake Tamari, lakini baada ya Kuzini naye, Mihemuko ya Ngono ilipoisha akamchukia Vibaya sana.

Kuna ujinga ambao shetani ameuhalalisha kwa vijana wa kizazi hiki, kuwa Upendo unadhihirishwa kwa tendo la NGONO, yaani bila kumuonjesha eti utakuwa hujakubali penzi lake, na wengine ukiwanyima eti wanaangua kilio nakusema “Darling mwenzio utaniua aaaaaa” , Mwambie kama kweli unanipenda basi kufa nione, utashangaa macho makavuu! anaendelea kula dagaa. KIJANA ANAYELILIA NGONO KABLA YA NDOA HAKUPENDI ANAKUTAMANI, na jambo la hatari kabisa ni kwamba anakutenganisha na Mungu wako kwa kukuingiza katika Dhambi – Neno linasema “Enyi Wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa Dunia ni kuwa ADUI wa Mungu? …” Yakobo 4:4. Iweni na akili, upendo unaokutenga na Mungu wako una faida gani? Ulimwengu utakapokugeuka na Tufani kuvuma juu yako, utamkimbilia nani kama sio Mungu?

Wito wangu kwa vijana wote wanaopenda kuwa na maisha yenye Baraka za mungu ni huu “Basi Mtiini Mungu, Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni Mungu naye atawakaribia ninyi ….” Yakobo 4:7-8. Mungu anahitaji vijana wanaoweza kumwambia Shetani “NO” au “HAPANA”, mpaka lini Shetani ataendelea kutawala maisha ya vijana? It is time to say “NO” and be ready because JESUS is around the corner. Mwisho nawapongeza vijana wote waliotangaza NIA ya kufunga Ndoa halali, na kuachana na Dhambi ya Uzinzi. Nitazidi kuwaombea ili Mungu azidi kuifanikisha mipango yenu.

NEEMA NA UPENDO WA MUNGU BABA UKAWE JUU YENU WOTE NA BARAKA TELE ZIKAAMBANE NANYI. NAWATAKIA WEEK END NJEMA.

Ev:  Eliezer Mwangosi.
0755808077 & 0652571733
Kwa masomo zaidi fungua mitandao ifuatayo: http://emwangosi.blogspot.com/ (Vijana) http://kayanafamilia.blogspot.com/ (Ndoa) http://matengenezo.blogspot.com/ (Ujumbe wa Matengenezo)

Thursday, March 8, 2012

JE UMEATHIRIKA NA KUTOTII WAZAZI?

 UJUMBE UNATOKA: Kutoka 20:12
Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako.

tAFAKARI:
Agizo la kuheshimu wazazi ni kati ya Amri kumi za Mungu, tatizo la watoto na vijana kutowatii wazazi linaendela kuwa sugu kila kunapokucha, si ajabu kusikia mtoto anaporomosha matusi ya Nguoni kwa baba au mama yake, mgeni akifika nyumbani utasikia mama anasema “nyie watoto mpishe mgeni akae” au “Amkia mgeni”, hiyo inaashiria nini? kwenye Mabasi utakuta Mama mja mzito amesimama huku watoto wa shule wamekaa, ni mara ngapi tunaona watoto wanafyonya watu wazima?. Wazazi wamepewa wajibu wa kuwa mawakili wa Mungu hapa duniani, hivyo ni lazima watoto watii na kuheshimu ushauri wa wazazi.

Angalia Mifano ifuatayo ya Vijana waliokaidi Ushauri wa wazazi wao na matokeo yake, kumbuka wazazi sio wale tu waliokuzaa ni watu wote wanaokuzidi Umri na wenye mamlaka juu yako.

1.      Kijana mmoja alikodi vijana wa kihuni kuja kumpiga baba yake, kwa sababu anamkataza kwenda Disko, mzee alivamiwa na kupigwa hadi mauti, hadi leo yule kijana ni kichaa, anayekula kwenye majalala ya taka.

2.      Binti mmoja alikuwa akionywa kuwa ni hatari kukaa faragha (kukaa na mwanaume katika chumba mkiwa wawili, au sehemu ya Giza), hata angekuwa mchumba wako, mtazini tuu. Binti alimuona mama yake amepitwa na wakati, akaamua kwenda kwa rafiki yake wa kiume, bila kutarajia alijikuta amezini, na hapohapo goli likafungwa, bahati mbaya alipomuambia kijana juu ya mimba yake, alimruka futi mia, mwisho wa yote yule dada akaamua kujiua kwa Sumu ya panya.

Kijana! kama umeamua kutozini, usijidanganye kuwa utashinda zinaa katika mazingira ya kukaa wawili chumbani. Uliona wapi wembe usinate kwenye Simaku vikiwa karibu? Au Ukalie jiko la Mkaa usiungue? Mapenzi ni moto mara moja, au umeme “transformer”. Kuna sehemu ambayo ukifika akili inapotea, kwa lugha ya kigeni inaitwa (Point of no Return), usijidanganye, wengi wamejikuta wana ukimwi, waja wazito, wameharibiwa usichana wao bila matarajio, kuishi au kuolewa na mtu asiyemtarajia n.k. kwa sababu ya kutozingatia ushauri huu.

3.      Kufungiwa nira na wasioamini, soma, 2Korintho 6:14-15. Hili ni tatizo sugu katika kizazi chetu, wala msije mkaiga jambo hili, Binti mmoja mkristo aliyekuwa amekaidi ushauri na kuamua kuolewa na Kijana wa Imani tofauti, alikutwa amefariki kwa kuwekewa sumu kwenye chakula, na mke mwenza ambaye hakutaka mume wake amuoe, ila kutokana na Imani ya mumewe kuoa wake wengi ilikuwa ruksa, hivyo akaoa na ndipo ugonvi ukaanza. Tunashuhudia matatizo mengi, ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kuabudu kwenye imani yako, watoto kukosa misingi ya Imani, Ndoa haiwi mwili mmoja tena kwa misingi ya Biblia, kwa sababu ya Imani, mwisho ni kujitenga na Mungu.

Mungu akikataza jambo, anamaanisha hivyo, usifanye, ukikaidi Mungu anasema, hata Maombi au sala yako ni CHUKIZO kwake “Yeye agauzaye sikio lake asiisikie sheria, Hata sala yake ni chukizo” Mithali 28:9. Unaweza kusema mbona naomba na ananiskia? Kumbuka hata mwizi anaomba anapoenda kuiba na anarudi salama, unafikiri nani anayejibu maombi? Na mwisho wake ni upi?

Kuna mashauri mengi kwa vijana ambayo tutaendelea kujifunza siku zijazo, ninachowaasa vijana ni kwamba msimjaribu Mungu kwa kufanya mambo aliyokataza, matokeo yake ni maangamizi ya kutisha yanayoujia Ulimwengu. Wale walio tayari wameathirika na kutosikia ushauri, ni wakati wao kumrudia Mungu, atawasamehe ili mradi waamue kuachana na njia za majuto. Waswahili wanasema "Asiyesikia la Mkuu huvunjika Guu" na "Majuto ni Mjukuu". Hebu Bwana atuangazie nuru yake ili tuwe na Amani sasa na hata milele.

NAWATAKIA SIKU NJEMA NA MAPUMZIKO MEMA YA MWISHO WA WIKI

Ev:  Eliezer Mwangosi.
0755808077 & 0652571733
Kwa masomo zaidi fungua mitandao ifuatayo: http://emwangosi.blogspot.com/ (Vijana) http://kayanafamilia.blogspot.com/ (Ndoa) http://matengenezo.blogspot.com/ (Ujumbe wa Matengenezo)

Wednesday, March 7, 2012

JE UNAWEZAJE KUPATA AMANI MOYONI?

UJUMBE UNATOKA:  ISAYA 48:17-18
Bwana, mkombozi wako, mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Mimi ni Bwana, Mungu wako, nikufundishaye ili upate FAIDA, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata. Laiti ungalisikiliza AMRI zangu! Ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya bahari.

tAFAKARI:
Siku za hivi karibuni nilimsikia kijana mmoja wa kiume akimwambia mwenzie akisema “Tafakari anayotoa huyu mzee mimi sitaki kuisoma, utafikiri ananisema mimi tu” moyoni nikacheka nikajifanya sijasikia,  na ni wengi wakifungua email zao wakiona tu NENO LA LEO wana “delete” hawataki hata kusoma, na wengine wanasoma ila hawazingatii.  Rafiki yangu kijana, Neno la Mungu ni Upanga unaogawanya Nafsi (Mwili) na Roho, ukiona unasoma neno linakukosoa, na linakuuma moyoni, mshukuru Mungu, hiyo ni sauti Mungu inakuonya, fanya uamuzi wa kutii neno lake. Ibilisi ndiye anayewaongoza watu kuchukia ukweli wa neno la Mungu ili baadaye awatese na hatimaye kuwaua kifo kibaya. Wewe mwenyewe ni shahidi ni faida gani umeipata kwa dhambi uliyoitenda? Ni kujilisha UPEPO usio na faida.

Katika tafiti zilizofanyika; Changamoto kubwa zinazowakibili vijana ni maswala ya Mahusiano yaani; Marafiki (Mapenzi), Uchumba na Ndoa. Swala hili la Mahusiano katika kizazi chetu cha sasa limekuwa na sula tofauti, zamani mtu akiingia kwenye mahusiano ilikuwa ni Baraka ya kudumu katika maisha, lakini siku hizi mambo yamegeuka, kijana akijiingiza kwenye mahusiano ni sawa na kubeba Bomu la Nuclear ambalo kila wakati anakaa kwa tahadhari hajui litapasuka lini. Vilio, Kuvunjika moyo, kukata tama, kuchanganyikiwa, kujiua, kujijutia, manung’uniko, makelele, magonvi, dhuluma, kuoneana, kuachana Solemba n.k. ndiyo sehemu ya maisha. Hata wanaofunga ndoa siku hizi, furaha zao ni za kitambo tu, baada ya hapo ni Majuto, kwa sababu mwanzilishi wa mahusiano yao ni Ibilisi aliyewaongoza kukidhi tama za miili yao, sio upendo wa Mungu.

Jambo la pili ni Ugumu wa Maisha, yaani kupata pesa za kutosha kupata mahitaji mfano. Kununua gari, kustarehe, kulipa pango, kujenga, kula, kuvaa, kulipa ada ya chuo n.k. Siku hizi kuna Majimama (Sugar Mumy) wenye pesa, vijana hawaoni wala kusikia, hata kama wanaogelea mabwawa marefu ya majimama, hawaangalii ili mradi mkono uingie kinywani, ikitokea wameoa vijana wenzao inakuwa ni usumbufu tu usiokoma. Hatuwasahau Majibaba wanaoitwa Mapedeshee, Mabuzi au ma ATM n.k. Vijana wa kike kutokana na maisha kuwa magumu wameamua kubeba hata mizigo isiyostahili yao. Binti mmoja alifiwa na Mwanaume kifuani akiwa anavunja Amri ya Uzinzi guest house, Kumbe buzi lenyewe gari lake ni afadhali gari la Mkaa, haliwaki mpaka uskume (kwa booster za kimasai).  Binti akiolewa na kijana naye inakuwa ni taabu, make alizoea kuendesha Magari ya Mizigo, halafu anajikuta anaendesha Bajaji au gari aina ya Epsi.

Vijana sio waaminifu kabisa, anakuwa na Wachumba, anakuwa na ATMs, na anakuwa na watu wa kula nao BATA. Hivi unategemea ndoa itakuwa na sura gani? Vijana! Katika tafakari ya leo, Mungu anasema “Mimi ni Bwana Mungu wako nikufundishaye ili upate FAIDA, Laiti ungelisikiliza AMRI zake, ndipo AMANI yako ingalikuwa kama mto wa MAJI na HAKI yako kama mawimbi ya Bahari”. Kijana unataka AMANI moyoni? Unataka FAIDA au Mafanikio katika mambo yako? Geuka sasa, mtazame Yesu Kristo, yatosha kumtumikia Shetani kwa maisha ya dhambi. Neema ya Yesu ipo kukuokoa na kukupatia Ushindi wa Dhambi.

MUNGU WA AMANI AWAPATIE SIKU NJEMA YENYE BARAKA TELE.

Ev:  Eliezer Mwangosi.
0755808077 & 0652571733