Monday, July 9, 2012

NI TAMU ILA NI SUMU


Ujumbe Unatoka: Ayubu 20:12-13, 27
Ingawa UOVU una tamu kinywani mwake, Ingawa auficha chini ya ulimi wake, Ingawa auhurumia, asikubali kuuacha uende zake, Lakini akaushika vivyo kinywani mwake….. Mbingu zitafunua wazi uovu wake, Nayo inchi itainuka kinyume chake. 

TAFAKARI:
 Ni hali ya kawaida katika ulimwengu wa maendeleo kuona vidonge hasa vya kutibu malaria kuona vimepakwa radha ya sukari kwa nje, lakini kwa ndani ni chungu ajabu. Siku moja niliona mtoto akilia baada ya kutafuna kidonge aina ya Comaquine ambacho alipolamba akaona ni kitamu akafikiri Pipi, baada ya kutafuna ndipo akakutana na Uchungu.  Ndivyo ilivyo kwa mitego ya panya, wengi wanaweka SUMU ndani ya Mchuzi wa Samaki au nyama, panya anapokula anasikia Utamu mpaka kwenye Kisogo, lakini baada ya muda mfupi utakuta amekufa bila matumaini.

Wewe kijana na rafiki yangu unayesoma tafakari ya leo, nataka nikuambie kuwa dhambi ni tamu lakini ndani yake Adui ameweka Sumu ambayo ni lazima itemize kusudi lake. Piga picha siku ulipokutana na huyo boy friend au girl friend wako, ukalegeza macho na kutamka neno “Honey / Sweet I LOVE YOU”  ulijisikiaje? Na hatimaye utakuta taratibu lakini kwa uhakika wanakokotana hadi wanaingia katika Dhambi ya Zinaa. Wengi hawapendi kuvunja Amri ya Mungu inayosema “USIZINI”, lakini kwa hila za shetani anawaangusha. Tendo la Ndoa nje ya Ndoa halali ni Dhambi ya Zinaa, hiyo ni sukari iliyotiwa sumu ya kufisha, inaua taratibu lakini kwa uhakika.  

Kijana mmoja aliyenusulika kufa akiwa amekunywa sumu ya panya akitaka kujiua baada ya kugundua ameambukizwa Virusi vya ukimwi, tulipomuuliza ilikuwaje? Akasema rafiki yangu wa kiume alinilazimisha kufanya naye ngono, siku moja alimtembelea boy friend wake, chumba chenyewe ni kimoja na viti ni kitanda, alipoingia, kwa maneno ya kubembeleza wakajikuta wamefika kwenye “Point of No Return” wakavunja AMRI sa saba, ndivyo vijana wengi walivyoanguka bila kutarajia na wanabaki wakisema “NINGEJUA” lakini wanakuwa wamechelewa.

Neno linasema, Dhambi ni TAMU na wengi wanajitahidi KUIFICHA ili wasigundulike, wasije wakaicha, Lakini Mungu anasema; Mbingu zitaifunua na  itawekwa wazi. Popote unapokuwa, iwe Guest House, Chumbani, kwenye vichochoro, hata iwe usiku wa GIZA nene, chochote unachofanya, Kamera ya Mbinguni inakumulika na kuchukuwa Picha, chicho la BWANA liko kila mahali likichunguza kila tendo – na mwisho anasema ATAUFUNUA UOVU HUO.

MUNGU ANATUFUTA VIJANA KAMA AKINA DANIEL KATIKA KIZAZI CHA LEO WATAKAOSIMAMA KWA UAMINIFU – KWA NINI USIWE WEWE?

SIKU YA LEO IKAWE YA BARAKA NA USHINDI TELE

Ev:  Eliezer Mwangosi.
Masomo zaidi:  http://emwangosi.blogspot.com/ (VIJANA) http://kayanafamilia.blogspot.com/ (NDOA) http://matengenezo.blogspot.com/ (UKWELI ULIOFICHIKA NA KUUKULIA WOKOVU)

MSIYACHOCHEE MAPENZI

Ujumbe unatoka:  Wimbo ulio bora 2:7 
Nawasihi, enyi binti  za Yerusalemu, kwa paa na kwa ayala wa porini, msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe”
TAFAKARI:
Kama kuna janga la HATARI ambalo jamii ilipaswa kulitangaza kwa siku za leo, ni Vijana kujihusisha na mapenzi kwa wakati usioruhusu. Katika tafakari za nyuma niliwahi kutoa somo la “Kila jambo lina wakati wake”. Swala la Mapenzi katika kizazi chetu limekuwa tishio, Kuna dada mmoja ambaye alikatisha masomo ya chuo kikuu kwa kuvurugikiwa na akili, kwa sababu ya mawazo mengi baada ya kuachwa na BOYFRIEND wake, hadi leo yuko nyumbani kama zezeta.

Mapenzi ni Moto ambao ukichochewa sio rahisi kuuzima mpaka utimize kusudi lake la kuteketeza, Mapenzi yanalewesha na kupiga upofu, ukinaswa na Upendo – Mtu Kipofu utaona ana makengengeza, Mwenye mapengo unaona ana Mwanya, yaani ukipenda hutaona Kasoro. Neno linasema “UPENDO una nguvu kama Mauti … Ni kama MOTO ambao hakuna maji yanayoweza KUUZIMA” Wimbo ulio bora 8:6-7. Ndio maana utakuta kijana anaogelea kwa Bibi kikongwe, hebu jaribu kumwambia huyo hakufai, atakuwa tayari kujiua, make yeye anamuona ni Binti wa Umri under eighteen.    

Ushauri wangu kwa Vijana ni Huu – Mungu ameweka Upendo ndani ya Mtu kwa makusudi ya KUDUMU, sio wa kuishia njiani au kuvunjika. Hivyo kabla hujaingia katika mahusiano ya Mapenzi na Mtu yeyote Mwambie Mungu akupatie the “Right Person at the Right Time”. Jamii yetu inaendelea kuathirika kwa ongezeko la Vijana wenye Misongo, inayotokana na vurugu za Mapenzi yasiyo na mpangilio. Shetani amefanikiwa kuteka vijana wengi – akiwatilia Sumu kwenye Sukali ya Mapenzi hata hawasikii ushauri.

Biblia inasema Ngono nje ya Ndoa ni UZINZI NA UASHERATI. Vijana asilimia kubwa wameziba masikio wasisikie neno la Mungu, naye Mungu anaziba masikio asisikie vilio vyao [Isaya 59:1-2] wanapokuwa wametelekezwa na matapeli wa Mapenzi. Bado Mungu anawataka vijana wafanye uamuzi upya wa kusimama Upande wake ili awapatie RAHA nafsini mwao sasa na hata Milele. 

VIJANA NAWAKIA SIKU NJEMA – MUNGU AWABARIKI NA KUWAPA AMANI

Ev. Eliezer Mwangosi

UJANA NI MAUA

NENO LA LEO:  Ayubu 14:1-2
“Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke, siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama vile UA, kisha hukatwa; hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe”
TAFAKARI:
Rafiki! Leo tunatafakari juu ya UA, wote tunajua kuwa UA LIKICHANUA KINACHOFUATA NI KUNYAUKA, na Jambo la kuvutia zaidi ni kuona linavyopendeza na kuvutia, mbali na wanadamu kupenda MAUA, hata wadudu pia utakuta wamejazana.
Maisha ya Mwanadamu ndivyo yalivyo, kama UA linavyonyauka ghafla ndivyo maisha yanavyokatika, kumbuka sisi sote ni marehemu watarajiwa wasiojua muda wa kifo.
Vijana! Mwisho wa UA kuchanua ni kunyauka, wengi huutumia wakati huo vibaya, HAWATULII, Utakuta Binti mzuri eti anajirusha na Libaba ambalo halina Mpango wa kumuoa ili mradi ana Vijisenti – Hao ni WADUDU WAHARIBIFU. Tunaona baadhi ya MAUA yanavyoharibiwa na wadudu waharibifu, yanatobolewa na kuchafuliwa, ndivyo vijana WANAVYOPOTEZEWA DIRA YA MAISHA. Akili zikiwarudia na kutaka Kuolewa au kuoa wanajikuta wamechelewa – UMRI WA KUCHANUA UMEPITA, hata wakitumia MAKE UP, hazisaidii, wadudu wote wamekimbilia maua mengine yanayochanua.
Vijana! Habari za ku “PASS TIME” na vija wenzenu kwa maisha ya Ngono, Ulevi, Muziki n.k. yanawapotezea DIRA ya Maisha, tumeshuhudia wengi wanasukumwa na TAMAA, na  Wengi wanatumika kama VYOMBO vya kukidhi tama za wengine, mwisho wake ni kuachwa kwenye Mataa. MAISHA YOYOTE YA DHAMBI NI TANZI YA UHARIBIFU.
VIJANA WENGI WANAJUTIA KWA YALIYOPITA NA WENGINE NDIO WAMEZAMA.
SULUHISHO NI KUMTEGEMEA MUNGU – KWAKE YOTE YANAWEZEKANA

NAWATAKIA SIKU NJEMA NA WEEK END NJEMA YENYE BARAKA TELE
Ev. Eliezer Mwangosi

SAMAKI AWA ATM

NENO LA LEO:  Mathayo 17:27
“Lakini tusije tukawakwaza, enenda baharini ukatupe ndoana, ukatwae samaki yule azukae kwanza; na ukifumbua mdomo wake utaona shekeli (Fedha); ichukue hiyo ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako”
TAFAKARI:
Watu wengi leo wanajiingiza katika vitendo vya uasi juu ya Mungu kwa sababu ya Maisha, tunaona: Ufisadi, Rushwa mpaka rushwa za Ngono, Ukahaba, Uongo n.k. ni sehemu ya maisha ya walio wengi. Wengi wako tayari wadhalilishwe ili mradi mkono uingie kinywani. Wapendwa Mungu yupo kwa ajili yetu, kwake hakuna lisilowezekana, wanaume wengi siku hizi wanasumbua mabinti na KADI  ZA ATM !  Angalia kisa cha Yesu akidaiwa Kodi, alimfanya SAMAKI kuwa ATM na Ndoano kuwa KADI ya kutoa Fedha (Shekeli), atashindwaje kukupatia mahitaji yako? Una jambo gani Gumu linalokusumbua? Mwambie Mungu hakuna asiloliweza.

Wapendwa tunaishi nyakati za Mwisho, siku za hivi karibuni kumezuka mjadala juu ya serikali yetu ya Tanzania kutofautiana na serikali ya Uingereza, baada ya kumkataa Balozi ambaye ameoa Mwanamume mwenzie. Swali kwa wengi ni hili, je ni kweli tutaweza kushinda vikwazo vya nchi tunazozitegemea? Mara zote katika maisha ni hatari kuishi maisha tegemezi, bila Mungu kuingilia kati juu ya jambo hili, sio rahisi kushinda mtego huu wa Shetani.

Ushauri wangu ni huu, pamoja na maamuzi yote tunayoyachukuwa kutetea maadili yetu, tunapaswa kuchukuwa hatua ya Kumrudia Mungu, kitendo cha kuupinga UOVU wa ushoga, tungali chini ya mamlaka ya Shetani kwa kutenda maovu mengine ni mchezo wa kuigiza. Ushoga ni Dhambi na ni machukizo kwa Mungu, neno la Mungu linasema “Usilale na Mwanamume  mfano wa kulala na Mwanamke; ni machukizo” Mambo ya Walawi 18:22.  Hivyo kufanya Ushoga au kukubaliana na Ushoga ni kujitia chini ya Laana ya Mungu.

WAPENDWA NI WAKATI WA KUUNGANA KUMUOMBA MUNGU ILI ATUPITISHE SALAMA KATIKA HAYA YANAYOUJIA ULIMWENGU

Na: Eliezer Mwangosi.