Thursday, December 29, 2011

MAWAZO YA MUNGU KWA VIJANA

Ujumbe wa leo unatoka – Yeremia 29:11,
“Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya AMANI, wala si ya mabaya, kuwapa ninyi TUMAINI, siku zenu za Mwisho”

TAFAKARI:
Vijana na Wazazi ambao ni washauri wa Vijana, inahitaji kutumia akili kidogo sana kuthibisha kuwa Ulimwengu wetu sasa uko taabani, angelikuwa ni binadamu tungesema yuko mahututi karibu kukata Roho. Hata hivyo Mungu anafanya kila njia ili watu waishi kwa AMANI na MATUMAINI katika hali ambayo wengi wamejikatia tama. Kuna usalama kusimama upande wa Mungu, zaidi ya hapo ni kukinywea kikombe – Siku ambayo Sukali itageuka kuwa dawa ya Mwarobaini au TAMU kuwa CHUNGU.

Leo nimeamua kujibu baadhi ya Maswali waliyoniuliza Vijana:
1.  Ni umri gani Mzuri wa kuoa au Kuolewa?
-          Kwa Mwanaume ni kati ya Miaka 25 hadi 35, na Mwanamke ni Miaka 20 hadi 30. Miaka hii ni wastani wa wanandoa kuwa na Muda mzuri wa Kuzaa, na kulea watoto hadi kuwasomesha, na hatimaye na wao kuanza maisha bila matatizo.
Watoto hawatakuita BABU au BIBI, Mwanamke utakuwa na Muda Mzuri wa Kuzaa, mtakuwa na nafasi nzuri ya kuzaa kwa mpango. N.K.

2.  Ni vizuri Mume na Mke wapishane miaka Mingapi? 
Kuna usemi vijana wanasema ng’ombe hazeeki maini na wengine wanasema “Age is just Numbers”. Vyovyote watakavyosema, kuna athari nyingi kama utaamua kuingia katika ndoa bila kujali Umri “Age Gape”. Ushauri wa kitaalamu na kisikolojia – wastani wa miaka ya kupishana ni Miaka Mitano hadi Kumi, Ibrahimu alimzidi Sarah Miaka Kumi [ Mwanzo 17:17 ].

-          Vijana mnaofugwa na Majimama (Sugar Mamy), mmtegwa kwa shida za maisha, kwani hata hivyo macho hayakomi kutamani maua yanayochipuka – Outing vipi inakubali? Kama ndio, hiyo ni ya kitambi muda si mrefu utamkimbia akiwa kibogoyo.
-          Na Mabinti wanaokubali  mizigo inayowazidi, yaani kuolewa na Wazee wana hasara kubwa, kuna siku Gari litazimika hata ukilisukuma halitawaka. Hiyo ni sawa na GARI LA MKAA KUWAPANDISHA WATALII, yaani ni kero tupu, wengi wanadanganywa na Vijisenti ambavyo mara nyingi havidumu.
Kuna maswali Mengi na Mashauri Mengi ila Muda hautoshi. Tutaendelea wiki ijayo na ninapanga kuwa na semina ya Ushauri kwa Vijana. Kumbuka Mungu anawawazia Mawazo ya AMANI katika Maisha yenu, ukimtegemea atakupatia Mwenzi wa kufanana naye.
MUNGU AWABARIKI NA KUWAPATIA SIKU NJEMA YENYE MAFANIKIO TELE
Ev. Eliezer Mwangosi

ATHARI YA ZINAA NA ULEVI

NENO LA LEO:  HOSEA 4:11
“Uzinzi na Divai na Divai Mpya huondoa fahamu za wanadamu”

tAFAKARI:
Watu wengi wanajiuliza; “Endapo kizazi chetu kitaendelea miaka 50 zaidi, hali ya maisha ya Mwanadamu yatakuwaje?”. Kwa kawaida Jamii yoyote yenye maadili ni matokeo ya Vijana Bora waliotangulia. Katika kizazi chetu cha sasa tunashuhudia Kuporomoka kwa MAADILI kuanzia Wazee, Vijana, hadi Watoto. Leo nimeona nikazie mambo mawili yanayochangia kuipeleka jamii yetu katika hali ambayo itamfanya Mungu aghaili Kumuumba mwanadamu kama ilivyokuwa wakati wa Nuhu na Sodoma.

Mungu anasema “ZINAA NA POMBE” ni mapacha wanaoshirikiana kuharibu akili za watu. Katika Kizazi chetu kuanzia Watoto, Vijana na hata Wazee wanakili kushindwa na Dhambi hii ya Zinaa na Pombe, hii ina maana wengi tayari hawana Ufahamu au AKILI. Uadilifu wa Kweli unatokana na Mtu kuongozwa na Mungu, sasa tutapata wapi Viongozi waadilifu kama watu wote ni Maadui wa Mungu kwa sababu ya Zinaa? Vijana wanakazana kwenda kwenye sehemu za IBADA, kumuomba mungu juu ya Masomo, Kupata kazi, Kupata Wachumba, kupata vipato vizuri n.k. Huku wanakili kushindwa na Zinaa ni Mungu yupi anategemewa ajibu maombi? Kwenda kumuomba Mungu, huku tunaendelea na dhambi ni Machukizo kwa mungu “Mithali 28:9, Isaya 59:1-2”, na Mwisho wake ni LAANA.

Sikilizeni wapendwa; Shetani ameamua kuharibu kizazi hiki kama alivyofanya Sodoma na enzi za Nuhu, Ndio maana amebuni Picha za Ngono, Mahaba / Mapenzi, Kukata Viuno Nusu uchi n.k. amezimwaga kwenye majumba yetu kwa njia ya TV na Mitandao ya Kompyuta na Simu, ili kuharibu akili za watu. Huwezi kushinda Zinaa kama kila wakati Unakodolea Macho Picha za Ngono au Mahaba. Hizo zinaamsha Ashiki za Mwili na kumfanya mtu awe na Pepo au Kichaa cha Uzinzi, wala hawezi kujizuia. Vijana kwa Wazazi wanaohitaji kuwa waadilifu wakiongozwa na Mungu, hawana budi kujitenga na kila uchafu unaoharibu Akili na hatimaye kuwatenga na Mungu.

Mungu anasema: “Iko Njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa Mtu; lakini mwisho wake ni njia ya MAUTI” Mithali 16:25. Ni swala la uamuzi kubadili Tabia, ni hakika inawezekana kwa kumtegemea Mungu, na kuondoa yasiyofaa machoni petu. 

BARAKA ZA BWANA ZIAMBATANE NASI SOTE SASA NA HATA MILELE - NAWATAKIA WEEKEND NJEMA

Ev:  Eliezer Mwangosi.

KIJANA KUISAFISHA NJIA YAKE

NENO LA LEO:  ZABURI 119:9
“Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako”

TAFAKARI:
Katika kizazi chetu, tunashuhudia waganga wa kienyeji wakipata umaarufu wa kupata wateja wengi, na moja ya tiba wanayotoa ni KUSAFISHA NYOTA, hii ina manisha kuondoa Mikosi, Nuksi n.k.

Dada mmoja alitoa ushuhuda wa mambo aliyofanyiwa na Fundi (Mganga wa Kienyeji) alipoenda kusafisha nyota ya Mapenzi – Tatizo lake lilikuwa kila akimpata Mwanaume anaishia kumtimizia haja ya Mwili baadaye anaachwa. Katika tiba ya kusafisha Nyota alifanyiwa Mambo ya aibu, ikiwemo kuchanjwa chale sehemu zake za Siri na kulazimika kufanya Ngono na huyo fundi ikiwa ni sehemu ya Tiba. Pamoja na yote hayo hakufanikiwa, mpaka alipojisalimisha Kwa Mungu. Hadi sasa baada ya maombi, Yule Dada ana Mume na watoto Ndani ya YESU.

Vijana wengi, wanahangaika kwa kukosa elimu ya Mungu, wanajiingiza katika mitindo ya maisha inayowatenga na Mungu wao, na mwishowe wanaishia kukata tamaa. Leo nahitaji kujibu baadhi ya Maswali niliyoulizwa na Vijana katika mfululizo wa masomo ninayotoa.

Swali: Je ni halali kuwa na wachumba zaidi ya Mmoja?
Jibu: Hapa kuna shida, huenda hata maana ya uchumba haieleweki, mchumba ni Yule ambaye tayari mmekubaliana na amekubalika na wazazi. Mahusiano mengine nje ya hayo sio uchumba. Mchumba ni mmoja tu, ni udanganyifu kuwa na wachumba wengi. Ukimtegemea Mungu atakupatia Mmoja anayefaa, kuliko kujiingiza katika mtego wa kumkubali kila anayeonekana, mwisho ya yote ni kujichanganya na wote kutoweka.

Swali: Nina Mchumba anataka TENDO la Ndoa kwanza kabla ya kuoana.
Jibu: Kama neno lilivyo, TENDO la NDOA ni kwa walio oana tu, ndiyo maana hakuna TENDO la UCHUMBA. Kitendo hicho nje ya Ndoa ni UZINIFU. Na Amri ya saba inasema “USIZINI” Kutoka 20:14. Athari za kufanya Ngono kabla ya Ndoa ni nyingi sana, Siku zijazo nitakuwa na mada hiyo tu. Matatizo katika ndoa za siku hizi asilimia kubwa yanatokana na Tendo la Ngono kabla ya Ndoa.

Swali: Muda unaenda Siolewi! Nifanyeje?
Jibu: Kuna sababu nyingi zinazosababisha mabinti wasiolewe, zikiwemo maisha aliyoyapitia huko Nyuma, kukataa wachumba katika muda muafaka n.k. pamoja na sababu zozote zile – Ukimtemea Mungu 100%, ninakuhakikishia kuwa Utaolewa. Jumapili ijayo tunapokea mahali ya Dada mwenye Umri wa Miaka 47 anaolewa na mwanaume wa miaka 48. Wote hawajawahi kuoa au kuolewa. Huwezi amini, lakini ndivyo. KWA MUNGU YOTE YANAWEZEKANA, BILA KUJALI YA NYUMA, TOA MAISHA YAKO KWA MUNGU NAYE ATAJIBU KWA WAKATI.

Swali: Sioni mwanamke wa Kuoa, nifanyeje?
Jibu: Wanawake wapo, ila huwaoni kwa sababu unatumia vipimo vya kibinadamu. Mwambie Mungu atakuletea Mwenzi wa kukufaa kwa Vipimo vya Mbinguni. Tatizo kubwa, Vijana wa kiume wanatawaliwa na TAMAA za ngono, hivyo wana ONJA ONJA na mwishowe wanaona wanawake wote walishaonjwa. Jambo la kushangaza ni hili – Wanadai mabinti sio waaminifu wakati wao wenyewe ndiyo wamewafikisha katika hali hiyo. Inakuwaje Mtu asiyemwaminifu anatafuta kuishi ni Mtu Mwaminifu? Huko ni kujichanganya.

USHAURI: Vinaja wa kiume na wa kike, wote mnafaa kuoa na kuolewa, ili mradi mmekubali kuzisafisha njia zenu. Tuna shuhudia Kahaba akimpokea Yesu baadaye anakuwa Mama wakufaa, mfano ni Mariam Magdalena alikuwa kahaba – alipokutana na Yesu pale kisimani – Alibadilika akawa kati ya wanawake waadilifu na BORA, waliofaidi mibaraka ya Mungu.   


VIJANA MUNGU AWABARIKI – AWAPATIE MAISHA MEMA


Na: Eliezer  Mwangosi

USHAURI KWA VIJANA

Ujumbe wa Leo:  1WaKorintho7:1-2
Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke. Lakini kwa sababu ya ZINAA kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe …..

TAFAKARI:   [Kwa Vijana na Wazee walio washauri wa Vijana]
1.    Ninahitaji kuoa lakini Maisha ni Magumu nifanyeje?
Ushauri: Ugumu wa maisha ni wimbo wa Taifa, unajua ni lini maisha yatakuwa Rahisi. Kuna mithali isemayo Mbuzi hula kulingana na urefu wa kamba yake, ili mradi unafanya kazi, kuna vitu vya msingi kuwa navyo kabla ya Kuoa (a) Uwe na chumba chako cha kulala nje ya Wazazi (b) Uwe na Kitanda na Godolo hata kama ni futi 3 (c) Uwe na uwezo wa kupata chakula – sio cha kuhemea (d) Uwe na uwezo wa kununua nguo. (e) Panga kufunga ndoa Rahisi, Gharama ya Ndoa peke yake bila Sherehe haizidi Sh. 20,000/=. Sherehe ya harusi sio lazima kama huna uwezo. (f) Usipende makuu na kushindana na wengine, ishi kulingana na uwezo ulio nao. (g) Uwe muwazi kwa mwenzio juu ya hali yako.

2.    Sioni Binti wa kuoa nifanyeje, karibu wote hawafai na sio waaminifu?
Ushauri: Mwambie mungu akupatie – Mke mwema mtu hupewa na Bwana, Mithali 19:14. Huoni mke anayekufaa kwa sababu unatumia akili yako. Mbona wengi unawatamkia unawapenda?.
Hata hivyo kuna madai juu ya mabinti yanayotakiwa ushauri: (a) Mabinti wanapenda Makuu / Expensive – Mwanaume usiwe muoga ongea nae, huenda ni katika harakati za kuji sop sop ili aonekane, pia mabinti angalieni muwe na kiasi katika kuremba, mnawaogopesha Waoaji. (b) Mabinti sio waaminifu -  Hili ni tatizo la wote wanaume na wanawake: Kama mwanaume kweli ni mwaminifu basi Tulia, Mungu atakupatia Mke mwema, lakini kama kuna sehemu unajituliza! – Ni kujidanganya kutafuta Binti Mwaminifu, Oa huyo unayejituliza kwake. Dawa ni wote kuwa waminifu (KUTOFANYA ZINAA KABLA YA NDOA).

3.    Wanaume wanatudanganya mabinti, wanatuchezea halafu hawaoi, tufanyeje?
Ushauri: (a) Usikubali kuchezewa, niliwambia, kati ya wanaume 10 wanaokutamkia wanakupenda, unaweza kubahatisha 1 anayekupenda kweli, wote wanasukumwa na tamaa ya mwili, ndivyo walivyoumbwa. Na kwa sababu mnawaruhusu kukata KIU ndio maana hawaoni haja ya kuoa. (b) Kama wewe binti ni Mwaminifu kabisa, tunda lako bado halijawahi kuliwa na wadudu waharibifu – Uwe na Subira, Mungu atakupatia Mwanaume atakayekufaa. Usidanganywe na wachumba FEKI wanaotaka Kuonja kwanza ili kuthibitisha kama kweli unawapenda. Sema kama Yusufu “Nitendeje ubaya huu ni mkosee Mungu?”.
Kwa mabinti wote waliopitia changamoto ya Kuchezewa na kuachwa, msikubali kuchezewa TENA, pamoja na kujiona mnakula STAREHE wote, baada ya hapo mwenye hasara ni Binti. Mpeni Mungu maisha yenu, atawasamehe yote mliyotenda, atawafanya viumbe vipya – Mtaolewa tu, kwa Mungu hakuna lisilowezekana.
Kwa wavulana wenye tabia ya UTAPELI WA MAPENZI, acheni tabia hiyo. Tabia ya kuonja onja, mtakuja kuonja SUMU ambayo mwisho ni Mauti. Kuna vijana ni hodari wa ku “TEST” utafikiri ni mafundi magari wanapima OIL. Toeni maisha yenu kwa Mungu na kuamua kuoa, Neno la Mungu linasema ni “Heri kuoa kuliko mwili kuwaka TAMAA”.

NAWATAKIA WEEK END NJEMA NA MAPUMZIKO MEMA
  
NB: Ukiwa na Swali lolote au changamoto yoyote ya maisha ya ujana, yaleteni kwa ushauri – Mungu ana majibu ya kila jambo linalomsumbua mwanadamu.
 
Ev:  Eliezer Mwangosi.

MTU ASIUDHARAU UJANA WAKO

Ujumbe unatoka:  1Timotheo 4:12 
Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi”
TAFAKARI:
Katika kizazi chetu DHARAU ni kitu cha kawaida, na katika mithali 14:21 Mungu anasema “Amdharauye mwenzake afanya dhambi”. Kuna watu ambao wanadharau wenzao kutokana na hali zao za maisha au maumbile, ambayo hawakupenda yatokee hivyo – Dharau ni Dhambi.

Somo letu la leo linahusu maisha ya Ujana, jana jioni nilipata kisa cha Binti aliyerudishwa kwa Mchungaji baada kufunga Ndoa na kukutwa usichana wake ulishaondolewa. Yeye alimhakikishia Mchumba wake kuwa hakumjua mwanamume, hivyo hata yeye alimkatalia katakata asifanye ngono wakati wa uchumba, kumbe alimdanganya akitegemea kurudisha usichana kwa dawa za Mchina. Piga picha ilikuwaje Ndoa ilipovunjika kwa namna hiyo! Ni wazi Binti alikuwa katika hali Ngumu na kujidharau nafsi. Lakini swali lilibaki kwa kijana, Je yeye alikuwa hajawahi Kuzini?

Neno la Mungu linasema “Akataaye maonyo huidharau nafsi” Mithali 15:32. Pamoja na sababu zote ambazo vijana wanazitoa wanapohalalisha Dhambi au kuvunja Maadili, mwisho wa yote ni kudharauliwa au kujidharau nafsi. Mungu anawataka vijana wawe kielelezo katika USEMI, MWENENDO, UPENDO, IMANI NA USAFI. Yaani; Lugha chafu, maneno ya kihuni, tabia za uhuni, wizi, ulevi, uongo, masengenyo, uchoyo, ubinafsi n.k. zinasababisha maisha ya kudharauliwa.

Familia nyingi zinalia kwa vijana kuishia kuvuta Bangi na madawa ya kulevya na hatimaye kuwa mateja na ombaomba, na wengine kuishia kuwa machangudoa. Vijana! shetani ni Mjanja, nia yake ni kuwatoa mikononi mwa Mungu ili awatawale na mwisho wa yote awatese.

Mabinti kaeni chonjo na Wavulana wanaohemea mapenzi bandia, watu hao ni HATARI, wakishaonja tu, siri zote wanazianika vijiweni kwa wenzao na mwishowe mabinti wanabaki kudharauliwa bila ya wao kujua. Ujana una thamani kubwa kwa Mungu na kwa jamii, hebu kila kijana AJITHAMINI, wekeni LUKU ya ROHO MTAKATIFU yenye uwezo wa kuzuia TAMAA ya mwili, kwa sababu kila DHAMBI INA MATOKEO YA MAJUTO MBELENI.
NAWATAKIA SIKU NJEMA NA MAISHA YENYE MAFANIKIO

Na: Eliezer Mwangosi

Thursday, December 8, 2011

UCHUMBA

SWALI JUU YA KUCHAGUA MCHUMBA
Swali: Nitajuaje kuwa anayenichumbia ni chaguo la Mungu? Make kuna wimbi la matapeli wa mapenzi?
Jibu:    Ukiwa mtoto wa Mungu, atakujulisha kuwa huyu ndiye, Mungu ana njia maelfu za kufunua yale Tusiyoyajua. Kinachotakiwa ni kukubali kuwa watoto wake ili tuisikie sauti yake, kama Baba anavyoongea na Mwanae ndivyo Mungu anavyojifunua kwa watoto wake.

Angalia mfano wa Mcha Mungu alivyompatia Isaka Mke aliyechaguliwa na Bwana, aliweka vigezo ambavyo Mungu alimuongoza Binti kuvitimiza, Isaka akajitwalia Mke wa kuchaguliwa na Bwana.
Mwanzo 24:13-14 [Kwa faida yako soma kisa kizima : Mwanzo 24:1-67]
“Tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji, na binti za watu wa mjini wanatoka kuteka maji, basin a iwe hivi; Yule msichana nitakayemwambia, tua mtungi wako, nakuomba, ninywe; naye akasema, unywe, nami nitawanywesha na ngamia zako pia; basi huyu na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka; na kwa hayo nitajua ya kuwa umemfadhili Bwana wangu”. Nina mifano Mingi ya namna hii.

NB: Jambo la kusikitisha, ndoa nyingi leo ni ndoano zilizotegwa na yule Adui ambaye ndiye mwanzilishi, hebu jiulize ni Mungu yupi anayehamasisha NGONO kabla ya Ndoa? Na siku hizi vijana wengi wanadai ku “test” kwanza ndipo wafunge Ndoa. Kwa hiyo wengi leo wamekuwa Mboga za kuonjwa na mwishowe kuishia kuachwa, lakini hata wakioana kwa mtindo huo wasipotubu na Mungu kuwasamehe, Ndoa haiwezi kuwa Salama, kwani anayeisimamia ni ADUI bila kujali sala za wachungaji. Amri inasema USIZINI. Anayeendelea na Dhambi Maombi yake ni Dhihaka kwa Mungu. Waebrania 6:4-6.

Vijana Mungu anawapenda na wakati wote anawawazia MEMA kwa siku zijazo, mnayoyaona ni furaha sasa hivi ni mashimo marefu ya siku za usoni katika maisha ya familia. Kubali Yesu atawale maisha yenu ili mpate kuishi maisha ya furaha na AMANI.

MUNGU AWABARIKI WOTE