“Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi”
TAFAKARI:
Katika kizazi chetu DHARAU ni kitu cha kawaida, na katika mithali 14:21 Mungu anasema “Amdharauye mwenzake afanya dhambi”. Kuna watu ambao wanadharau wenzao kutokana na hali zao za maisha au maumbile, ambayo hawakupenda yatokee hivyo – Dharau ni Dhambi.
Somo letu la leo linahusu maisha ya Ujana, jana jioni nilipata kisa cha Binti aliyerudishwa kwa Mchungaji baada kufunga Ndoa na kukutwa usichana wake ulishaondolewa. Yeye alimhakikishia Mchumba wake kuwa hakumjua mwanamume, hivyo hata yeye alimkatalia katakata asifanye ngono wakati wa uchumba, kumbe alimdanganya akitegemea kurudisha usichana kwa dawa za Mchina. Piga picha ilikuwaje Ndoa ilipovunjika kwa namna hiyo! Ni wazi Binti alikuwa katika hali Ngumu na kujidharau nafsi. Lakini swali lilibaki kwa kijana, Je yeye alikuwa hajawahi Kuzini?
Neno la Mungu linasema “Akataaye maonyo huidharau nafsi” Mithali 15:32. Pamoja na sababu zote ambazo vijana wanazitoa wanapohalalisha Dhambi au kuvunja Maadili, mwisho wa yote ni kudharauliwa au kujidharau nafsi. Mungu anawataka vijana wawe kielelezo katika USEMI, MWENENDO, UPENDO, IMANI NA USAFI. Yaani; Lugha chafu, maneno ya kihuni, tabia za uhuni, wizi, ulevi, uongo, masengenyo, uchoyo, ubinafsi n.k. zinasababisha maisha ya kudharauliwa.
Familia nyingi zinalia kwa vijana kuishia kuvuta Bangi na madawa ya kulevya na hatimaye kuwa mateja na ombaomba, na wengine kuishia kuwa machangudoa. Vijana! shetani ni Mjanja, nia yake ni kuwatoa mikononi mwa Mungu ili awatawale na mwisho wa yote awatese.
Mabinti kaeni chonjo na Wavulana wanaohemea mapenzi bandia, watu hao ni HATARI, wakishaonja tu, siri zote wanazianika vijiweni kwa wenzao na mwishowe mabinti wanabaki kudharauliwa bila ya wao kujua. Ujana una thamani kubwa kwa Mungu na kwa jamii, hebu kila kijana AJITHAMINI, wekeni LUKU ya ROHO MTAKATIFU yenye uwezo wa kuzuia TAMAA ya mwili, kwa sababu kila DHAMBI INA MATOKEO YA MAJUTO MBELENI.
NAWATAKIA SIKU NJEMA NA MAISHA YENYE MAFANIKIO
Na: Eliezer Mwangosi
No comments:
Post a Comment